Monday, March 25, 2013
MBINU ZA KUMUWEZA, MWANAMKE ALIYE MGUMU KUTONGOZEKA
wakati mwingine, vitu huweza kumaanisha zaidi ya tuwezavyo kutamka kwa vinywa vyetu
MWANAMUME yeyote anapotaka kumtongoza mwanamke hulazimika kwanza kumwonesha – japo kwa matendo – kuwa anampenda, au kwamba amevutiwa naye, hata kama ni kimwili tu. Hatua hii ndiyo yenye changamoto kubwa zaidi kwa mwanamume, maana ndipo wakati anapokuwa anajaribu kufikisha ujumbe kwa mlengwa huku yeye mwenyewe akijihakikishia kuwa haharibu mambo.
Mwanamume anapokuwa anajaribu kufikisha ujumbe wa “nakupenda” kwa mwanamke, mapigo ya moyo yanaweza kumwenda mbio, hususan kama mwanamke mwenyewe anaonekana kuwa “maji marefu”. Hata hivyo, ni kazi ambayo kila mwanamume hulazimika kuifanya.
Kazi hii ya kufikisha ujumbe kwa mara ya kwanza huhitaji umakini. Bahati njema, shughuli yenyewe ina sayansi yake, ambayo ina misingi katika mahusiano ya kijamii. Ukifahamu sayansi hii inaweza kuwa rahisi zaidi kwako kufikisha ujumbe kwa mtarajiwa wako – na kufanikiwa.
1. KUKUTANISHA MACHO NI MUHIMU
Kawaida, mambo yote huanzia – na pengine kuishia – katika kukutanisha macho. Mwanamke atakapobaini kuwa hujajaribu kumwangalia japo kwa sekunde mbili mfululizo, ataondoa mawazo na hisia zake kwako hata kabla hujasema neno lolote.
Macho ndizo zana muhimu zaidi mtu anapokuwa anataka kufikisha ujumbe kwa mwenzake kuwa anampenda, au amevutiwa naye. Hii ni kwa sababu macho ndiyo vipitisho na visambazaji muhimu vya ishara baina ya mtu na mtu, hata kama si katika masuala yanayohusiana na mapenzi.
Kukutanisha macho na mtu wa jinsia nyingine unayevutiwa naye au anayevutiwa nawe ni jambo lenye nguvu za ajabu katika kuanzisha uhusiano. Kwa sababu hiyo, hata unapofanikiwa kumtazama moja kwa moja machoni mwenzako hutarajiwi kutumia zaidi ya sekunde mbili, kutokana na nguvu iliyomo katika mawasiliano haya.
Katika hili, wanaume mahiri hufahamu ni wakati gani wa kumwangalia mwanamke na ni wakati gani wa kutomwangalia. Mara nyingi, ni vizuri zaidi kumwangalia zaidi mwanamke wakati anapozungumza, huku ukikwepesha macho kidogo pale unapozungumza wewe.
2. UNATAKIWA UWIANO, UKWELI KATIKA MAZUNGUMZO
Ni jambo lisilopingika kwamba wanaume na wanawake wanatofautiana katika maana ya dhana ya mawasiliano. Hata hivyo, bado inawezekana kuendesha mazungumzo shirikishi na yenye kuburudisha ukiwa na mwanamke, bila kuonekana wa bandia.
Watu wa jinsia zote mbili wanaweza kutuhumiwa kwa kupindisha ukweli na kujaribu kuficha tabia na mienendo yao wanapozungumza na wapenzi watarajiwa. Naam, katika mazungumzo ya kwanza baina ya wapenzi au wachumba watarajiwa uwongo – ukiwemo ule usiotarajiwa – huwa mwingi.
Katika mazungumzo ya kwanza ni kawaida kwa mwanamume kubadilisha matendo yake na mtindo wake wa kuzungumza kwa maslahi ya kumpata mwanamke, jambo ambalo huifanya hulka yake ya wakati huo kuwa ya bandia. Lakini pia wasichana/wanawake husema “Nakupenda” bila kumaanisha, pengine kwa ajili ya kumfurahisha mwanamume, au kusikia mwanamume atasemaje.
Jambo la muhimu katika mazungumzo ya awali baina ya mwanamume na mwanamke ni kuepuka michezo ya kudanganyana na kukwepana, badala yake, yafanye mazungumzo kuwa rahisi na halisi. Hapo ndipo mwanamume hujitofautisha na wanaume wengine na kupendwa kwa sababu hiyo.
3. USIPUUZE NGUVU YA LUGHA YA MATENDO
Wakati mtu anapokuwa akijaribu kuwasilisha ujumbe wa “Nakupenda” kwa mwenzake, lugha ya matendo yake huzungumza kwa sauti kubwa zaidi kuliko maneno yake. Hili limeweza kuthibitishwa kwa nyakati mbalimbali kutokana na tafiti mbalimbali.
Katika muktadha wa kujaribu kufikisha ujumbe wa “Nakupenda” kwa mlengwa, lugha ya matendo ndiyo yenye nafasi kubwa zaidi. Kwa hakika, asilimia kubwa ya ujumbe unaowasilishwa kwa mlengwa huwasilishwa kwa njia ya matendo ya mwili na si maneno. Ni asilimia ndogo tu ya ujumbe inayowasilishwa kwa maneno – na wakati mwingine maneno huweza kuleta matatizo maana katika kuzungumza kuna kujikwaa kwingi, kwani ulimi hauna mfupa.
Ili uweze kufanikiwa katika kueleza nia yako kwa mwanamke, lazima ujue jinsi ya kutumia lugha ya matendo yako. Na pengine hutatumia nguvu, maana watu husema penzi kikohozi – kama unalo litaonekana tu machoni pa mlengwa.
Ukitafakari kwa makini utabaini kuwa huhitaji kusema sana ndipo uweze kupendwa, kwani maneno huchangia asilimia kidogo tu. La muhimu ni kuhakikisha kuwa mlengwa wako anakusoma na kukuelewa vizuri kwa kuangalia matendo ya mwili wako.
4. ACHA ASILI ICHUKUE MKONDO WAKE
Katika nadharia mbalimbali za kijamii na kidini ni jambo la kawaida kusikia kuwa binadamu wote ni sawa. Hata hivyo, katika muktadha wa kimapenzi, kila mtu mmoja mmoja anafahamu kabisa kuwa si kila mwanamume/mwanamke ni sawa na mwenzake.
Methali yenye asili ya kimagharibi husema “Uzuri wa mtu uko katika macho ya yule anayemtazama.” Hii ina maana pia kwamba, kila mtu anavyo vigezo vyake vya uzuri kwa kuzingatia maumbile yake. Pia jamii zinavyo vigezo vya uzuri, lakini hutangulia kwanza vigezo binafsi.
Unapokuwa umekaa na mwanamke ambaye anakuvutia kwa mwonekano wake, sauti yake na kadhalika, si rahisi sana kujizuia kuonesha kuwa anakuvutia. Hii ni kwa sababu si wewe, bali ni nafsi yako inayokusukuma. Na yeye mwenyewe atakusoma kwa kuangalia lugha ya matendo yako na kukwelewa, utakaobaki ni uamuzi wake tu.
Katika jamii kuna vigezo kuhusiana na kiuno, miguu, maziwa, makalio na kadhalika. Wengi wa wanajamii huvizingatia na kuongeza vyao. Huu ni ukweli wa kibiolojia ambao hauwezi kupingika. Mwanamke mwenye vigezo vinavyokubalika zaidi katika jamii yake atawavutia wanaume wengi zaidi. Hapa mwanamume hahitaji kutumia nguvu nyingi – asili ya maumbile itamsaidia humtambulisha mwanamke kuwa amempenda.
5. TUMIA CHANGAMOTO YA WALAKINI
Mara nyingi changamoto kubwa katika suala zima la mtu kubainisha nia yake kwa mwanamke hutokana na ukweli kwamba katika mchakato mzima huwa kuna wasiwasi na walakini. Kwa hakika, jambo hili ni la “pengine” au “labda” kutokana na kutoweza kufahamu kirahisi mwenzako anawaza nini.
Unapoonesha nia yako ya kumpenda mwanamke, ni kama unaamsha hisia zake kwako na ni kama vile unamuuliza: “Ungependa kuwa nami?” Kwa njia hii ni kama utakuwa unafungua mlango wa kupata jibu la “ndiyo” au “hapana” kwani huyo unayemwonesha kuwa unampenda na yeye ana matakwa yake na mapendeleo yake.
Kimsingi hakuna kanuni wala sheria rasmi unazopaswa kuzingatia wakati wote. La muhimu ni wewe mwenyewe kujiachia na kuingia katika maji usiyofahamu kina wala mwisho wake, bali wewe nenda na mkondo wake huku ukitarajia kuwa lolote linaweza kutokea. Hiyo ndiyo sehemu ya raha yake.
6. DHIBITI HISIA, MIHEMKO
Tofauti na mwanamke, mwanamume anayejaribu kuonesha nia yake hatakiwi kujiweka katika mkao wa mwanamitindo. Wanawake ndio hufahamika zaidi kwa mikao yao “ya kula” wanapokuwa katika mawindo (japo wengi hubisha), lakini si mwanamume. Wanawake ndio hutarajiwa kujieleza zaidi kwa njia ya matendo na mikao, lakini wanaume hutarajiwa kudhibiti hisia na mihemko yao .
Tofauti katika lugha ya matendo baina ya watu wa jinsia mbili hutokana na maumbile ya kujenetiki pamoja na utamaduni wa jamii husika. Yote yakizingatiwa, matakwa ya mwanamke ndiyo hupewa kipaumbele zaidi. Kwa ufupi, matendo ya kutongoza ya mwanamke huwa wazi zaidi, lakini mwanamume hulazimika kuficha hisia na mihemko yake.
IFAHAMU SAYANSI HII
Wajibu wa kufikisha ujumbe kwa mtu wa jinsia tofauti ni wa kila mmoja – mwanamume na mwanamke. Hata hivyo, wanaume ndio wenye jukumu kubwa zaidi la kuanzisha, kwa kuzingatia utamaduni wa jamii nyingi. Unaweza ukaona ugumu, lakini ipo sayansi itakayokusaidia. Kama una wasiwasi na uwezo wako, ni vizuri kuyazingatia yote yaliyobainishwa hapa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Duh nimekubali mtuwangu sayansi hii ni muhimu sana kama mm ndio kwaaanza nimeamka.....
ReplyDeleteAsante mdau,kukumbushana ni muhimu sana.
Delete