Tuesday, March 12, 2013
KUAMINIANA NI NGUZO KUU KATIKA PENZI
Nina uhakika baadhi yetu tuna wapenzi ambao wako mbali, hilo lisikupe shaka. Bado unaweza kuendelea kuliboresha penzi lako na mwisho kutimiza ndoto zenu mlizojiwekea za aidha kuoana kwa wale ambao bado wapo wapo au kudumisha ndoa yenu kwa ninyi mliooana.
Katika hili kuna mambo mawili ya msingi ambayo leo nataka
kuyazungumzia ili kuhakikisha uhusiano wenu hautetereki.
Kwanza, hakikisha humsaliti mpenzi wako. Ukitaka kufurahia mapenzi, lazima usiwe msaliti. Upo msemo usemao, ukimsaliti mpenzi wako ujue nawe utasalitiwa, sasa ili uepukane na hilo ni vyema ukajiwekea dhana ya uaminifu wewe kama wewe kwanza.
Jisemee mwenyewe; “Kwa nini nimsaliti mpenzi wangu? Nampenda sana na najua nikimsaliti hatajua, lakini na yeye akinisaliti je?” Tafakari maneno hayo kwa makini sana, naamini kuna kitu utajifunza.
Jichunge mwenyewe, usikubali kabisa kuharibu thamani yako kwa kumruhusu mtu mwingine aujue mwili wako kwa kuwa tu umesikia ‘hamu’.
Kumbuka mwili wako ni kwa ajili ya mpenzi wako pekee, endelea na dhana hiyo siku zote utakazokuwa mbali naye, naamini utafurahi!
Kwa kufanya hivyo, hutaona faida yake kwa haraka lakini fikiria hili kwa makini, kama wewe umeamua kuwa mwaminifu kwa mwenzi wako kwa kutambua thamani yake, kwa nini Mungu asikulindie huko alipo? Ila lazima ufahamu jambo moja, Mungu anaweza kukulindia mwenzi wako ikiwa naye anakupenda kwa dhati na ana nia ya kuishi na wewe hapo baadaye.
Jambo lingine la msingi ni kujenga uaminifu kwake. Baada ya kuhakikisha kwamba humsaliti, sasa ni wakati wako wa kuhakikisha unamwamini katika kiwango cha mwisho. Usimwoneshe mashaka sana na nyendo zake. Wakati mwingine unaweza kumpigia simu asipokee, hilo lisikuchanganye.
Kuna baadhi ya watu, akimpigia simu mpenzi wake akiona hajapokea, tayari hisia zake zinakuwa mbali na muda huo huo anamwandikia meseji mbaya za ukali na kumtuhumu kwamba anajua huko aliko anamsaliti! Huna haja ya kufanya hivyo, onyesha kumwamini.
Kama umempigia na simu yake haipatikani, ni wakati wako wa kumwandikia meseji ya kumpa pole kwa kazi kutokana na kutambua kwako kwamba muda huo alikuwa bize.
Mwandikie hivi; “Natambua ni majukumu mengi uliyonayo muda huu ndiyo yaliyosababisha ushindwe kupokea simu yangu, usijali kwa hilo. Nakupenda sana na natambua kwamba mimi ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha nakuwa karibu na wewe kwa kila kitu, nakupenda mpenzi wangu, kazi njema.”
Ujumbe huo utamfurahisha, kama alikuwa na nia ya kukusaliti, hawezi kufanya hivyo kwani atakuwa anajua anamsaliti mwenzi ambaye anamwamini katika kiwango cha mwisho.
Kumuamini kwako kutamfanya aone ni jinsi gani ambavyo wewe mwenyewe unavyojiamini na usivyo na wazo la kumsaliti! Kwa nini yeye akufanyie hivyo? Lazima atabadilisha wazo lake.
Mpenzi msomaji wangu, hayo ni mambo mawili ya msingi ambayo unatakiwa kuyazingatia pale unapokuwa mbali na mpenzi wako. Kumbuka kuwa mbali na huyo uliyetokea kumpenda haiwezi kuwa sababu ya nyie kutengana.
Mtatengana tu endapo hakuna mapenzi ya dhati kati yenu lakini kama mmependana kiukweli kutoka mioyoni mwenu, hata muwe mbali kwa muda mrefu kiasi gani, bado hakuna cha kuliua penzi lenu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Mawazo yako ya busara na yana nguvu ya ajabu,inamjenga mtu kuwa mstaarabu wa kiwango cha juu sana kwa kuwaza mema na si mabaya.Endelea kutuwekea mbinu mbalimbali kama hizi maana hakuna mahala pengine pa kujifunza mambo haya. Mungu akubariki. By Danny Ezekiel E-mail:dannymtalii@yahoo.com Hotline: 0757 646 381.
ReplyDelete